Ufaransa yaeleza wasiwasi kuhusu hali Burundi
Ufaransa imependekeza hatua zichukuliwe kusitisha mauaji ambayo yamekuwa yakiendelea nchini Burundi.
Taifa
hilo liliwasilisha mswada wa mapendekezo kwa Baraza Kuu la Usalama la
Umoja wa Mataifa Jumatatu likieleza wasiwasi wake kutokana na machafuko
yanayoendelea nchini humo.
Machafuko hayo ndiyo mabaya zaidi nchini humo katika kipindi cha miaka kumi.
Ghasia
zilianza Aprili baada ya maandamano ya kupinga hatua ya Rais Pierre
Nkurunziza kutangaza angewania urais kwa muhula wa tatu. Jumamosi,
watu tisa waliuawa kwa kupigwa risasi katika baa moja mji mkuu wa Bujumbura.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alishutumu mauaji hayo ya Jumatatu na kusema mmoja wa waliouawa alikuwa afisa wa UN.
Afisa
mmoja wa polisi anadaiwa kujeruhiwa na takriban watu wawili kuuawa huku
polisi wakindelea kusaka silaha katika nyumba za wakazi mitaa ambayo ni
ngome ya wapinzani.
Rais wa Rwanda Paul Kagame
amekosoa viongozi wa Burundi kutokana na wanavyoshughulikia mzozo
nchini humo na kuna wasiwasi huenda kukatokea mauaji ya kimbari,
mwandishi wa BBC Alastair Leithead anasema.
Naibu balozi wa
Ufaransa katika UN Alexis Lamek aliambia AFP kwamba Ufaransa
“imehofishwa sana na yanayoendelea Burundi kwa sasa.”
Ujumbe wa Ufaransa katika UN ulisema mashauriano kuhusu azimio lake yangeanza Jumatatu jioni.
Shirika
la International Crisis Group lenye makao yake Brussels limeonya kuwa
lugha inayotumiwa kwa sasa Burundi “inashabihiana sana” na iliyotumiwa
Rwanda kabla ya mauaji ya halaiki ya 1994.
Machafuko yalianza
Aprili Nkurunziza aliposema muhula wake wa kwanza wa urais haukufaa
kuhesabiwa katika kutekeleza takwa la kikatiba la rais kuhudumu mihula
miwili pekee kwa kuwa alichaguliwa na wabunge wakati huo.
No comments:
Post a Comment