MAZINGIRA

JUE BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO TANZANIA [TADB]

Katika juhudi za kuinua ukuaji wa uchumi na Kupunguza umaskini nchini Tanzania, Serikali imechukua hatua mbalimbali zikilenga kuharakisha mapinduzi na maendeleo katika Sekta ya Kilimo, ambayo ina ajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya Tanzania.

Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa sekta ya Kilimo, bado ukuaji wa sekta hiyo umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbali mbali kama vile kiwango kidogo cha uzalishaji; ukosefu wa mbinu na teknologia za kisasa; matumizi madogo ya umwagiliaji; ukosefu wa mtaji na upatikanaji wa mikopo kwa wakulima; ukosefu wa masoko ya mazao na yasiyotosheleza; ufinyu wa bei za mazao; miundo mbinu mibovu ya usafirishaji; maghala ya kuhifadhi mazao; nishati ya umeme na miundombinu hafifu ya ya vijijini; ufinyu au kutokuwepo kwa ongezeko la thamani kwa mazao ya kilimo; mabadiliko ya hali ya hewa; na mmomonyoko wa udongo.

Changamoto hizo hapo juu, zikiambatana na ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya maendeleo ya Kilimo nchini Tanzania na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa kwenye upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa; mikopo ya muda mfupi mfupi; masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa; sekta ya kilimo imekuwa ikikosa mikopo ya kutosha kuendeleza kilimo chenye tija kwa mkulima/wakulima nchini.

Kutokana na changamoto tajwa hapo juu, Serikali imeamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuweza kuwezesha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuhamasisha taasisi zingine za fedha nchini kusaidiana na Benki Kuu ya Tanzania kuongeza kiasi cha kutoa mikopo katika sekta ya kilimo ili kuwezesha mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Kilimo. TADB kwa sasa iko tayari baada ya kukamilisha masharti yanayotakiwa na Benki Kuu ili kupatiwa leseni ya kudumu kuanza shughuli zake rasmi baada ya kuzinduliwa tarehe 8.8.2015.

No comments:

Post a Comment