Rais Vladimir Putin wa Urusi ameilaumu Jumuiya ya Kujihami ya
NATO kwa kile alichokiita "matamshi makali" na "harakati zake za
uchokozi" karibu na mpaka wa Urusi. Rais Putin ameonya visa kama hivyo
vitailazimisha Moscow kuimarisha nguvu zake za kijeshi. "NATO inazidisha
maneno na harakati za uchokozi karibu na mipaka yetu," amesema Rais
Putin mbele ya wabunge wa nchi hiyo waliokusanyika katika kumbukumbu za
miaka 75 tangu Ujerumani ya zamani ya Wanazi ilipoivamia Usovieti. Rais
Putin amezikosoa nchi za Magharibi kwa kukataa mchango wa Urusi kusaidia
kukabiliana na adui wa pamoja ambae ni ugaidi wa kimataifa, kama
walivyolipuuza onyo la Soviet Union kuhusu Hitler na kama wanavyojaribu
kuitenga Moscow katika mzozo wa Ukraine. Uhusiano kati ya Urusi na nchi
za Magharibi umepooza na kufikia kiwango cha vita baridi tangu Moscow
ilipolikalia eneo la Crimea mwaka 2014 na kuunga mkono vuguvugu la
wanaotaka kujitenga mashariki ya Ukraine.
No comments:
Post a Comment