Tuesday, 14 June 2016

DIRISHA LA USAJILI KUFUNGULIWA RASMI KESHO


DIRISHA la usajili kwa wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) na ligi Daraja la kwanza (FDL) litafunguliwa rasmi kesho huku timu zikishauriwa kufanya usajili kwa umakini mkubwa na linatarajiwa kufungwa Agosti 6 ambapo usajili huo utaenda sambamba na semina elekezi kwa viongozi wawili wa timu zinazo shiriki ligi kuu, ligi daraja la kwanza pamoja na ligi daraja la pili na  wanaotakiwa kuhudhuria semina hiyo ni Katibu mkuu wa klabu pamoja na Afisa usajili.

 Afisa habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Alfred Lucas amesema kuwa semina hiyo itahusu matumizi ya mifumo ya usajili kwa njia ya mtandao (TMS) kwani msimu ujao ni lazima kila timu iwasilishe usajili wa wachezaji wake kwa mfumo wa TMS kama FIFA walivyoelekeza.

"Misimu miwili iyopita tulianza kuutumia mfumo huu lakini haujaonesha kufanikiwa sana na ndio maana imeitishwa semina hii kwani kwa msimu ujao wachezaji watakaotambuliwa ni wale watakaosajiliwa kwa mfumo wa TMS", amesema Alfred. Semina hiyo itaanza siku ya jumatatu semina itakayowahusu viongozi wa ligi kuu, Jumanne itakuwa kwa ajili wa viongozi wa Ligi daraja la kwanza huku ikimalizika kwa viongozi wa ligi daraja la pili siku ya Jumatano.

Kuanzia leo hadi Juni 30 kutahusisha uhamisho wa wachezaji huku timu hizo pia zikitakiwa kuweka wazi wachezaji wanaowaacha  ili waweze kusajiliwa na timu nyingine endapo wanawahitaji. Kipindi cha Agosti 7 hadi 14 kitatumika kwa ajili ya mapingamizi kabla ya kuthibitisha usajili kwa hatua ya kwanza kati ya Agosti 15 na Agosti 19, huku hatua ya pili ikianza Agosti 17 hadi Septemba 7. 

Na pingamizi la hatua ya pili zitaanza  Septemba 8 hadi Septemba 14 na Septemba 15 hadi 17 itakuwa ni kipindi cha kuthibitisha usajili hatua ya pili.

TFF pia imezitaka klabu zinazoshiriki ligi kuu (VPL), ligi daraja la kwanza (FDL) pamoja na daraja la pili (SDL) kutaja viwanja vyake vya nyumbani kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Timu hizo zinatakiwa kuwasilisha taarifa ya viwanja watakavyovichagua kabla ya Juni 20 mwaka huu.

Klabu hizo zinatakiwa kupeleka vipimo vya viwanja husika ili TFF kupitia kamati ya mashindano ijiridhishe kama vitafaa kutumika kwa ajili ya ligi husika na timu zinazoshiriki mashindano hayo pia zinatakiwa kuambatanisha vipimo hivyo na aina ya nyasi, idadi ya vyumba, uwezo wa mashabiki wanaoweza kuingia pamoja na jina la mmiliki.

"TFF itahitaji kupata taarifa mapema na iweze kufanyia kazi kwani ni muhimu kukagua viwanja hivyo kama vina sifa zinazostahiki na hata kama ikitokea mechi zimepangwa usiku basi timu ziweze kucheza", amesema Alfred.


Tumezielekeza kwamba iwapo timu haina uwanja wa nyumbani unaofaa kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom inaweza kuchagua uwanja mwingine katika mji au mkoa wa jirani. Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (3) Ligi Kuu Tanzania Bara toleo la 2016/17.

No comments:

Post a Comment