CCM YAWASILISHA KWA MSAJILI WA VYAMA MATUMIZI YA UCHAGUZI MKUU
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) leo kimewasilisha kwa Msajili wa Vyama, hati zake
za gharama ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana, na kuwa chama cha
pili kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini.
Ujumbe wa CCM uliongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa CCM, Stanslaus
Mamilo na Mwanasheria wa CCM Adamson Sinka na kuwasilisha hati na
vielelezo vya matumizi hayo kwa Mwangalizi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama,
Mkuu wa Masijala Galasia Simbachawene.
Akikabidhi hati na vielelezo hivyo Mamililo alisema, CCM imelichukua
swala hilo umuhimu mkubwa ndiyo sababu imefanya hivyo ndani ya wakati
kwa kuwa mda wa kuwasilisha matumizi ya gharama za uchaguzi kwa wagombea
na vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 2015, ni
Juni 25, 2016.
"Sisi hatuwezi kuwa kama vyama vingine kwa kuwa ni Tasisi kubwa ambayo
haina budi kufuata kanuni, taratibu na sheria za nchi hasa ikizingatiwa
kwamba CCM ndiyo chama tawala hivyo lazima kionyeshe mfanomzuri ili
kiendelee kuwa chama cha kuigwa ", alisema Mamilo.
Mamililo aliwasilisha hati na vielelezo vya matumizi ya Chama na
wagombea wa nafasi mbalimbali kupitia CCM ikiwemo Urais, Wabunge na
Madiwani.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa hati na vielelezo hivyo, Galasia
alisema, katika vyama vyote vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu uliopita
ni CCM na ACT-Wazalendo ndivyo ambavyo tayari vimekamilisha bila
shuruti sheria ya kuwasilisha gharama zake za uchaguzi.
Alisema, uwasilishaji wa gharama hizo ni muhimu sana kwa kuwa ni suala
la kisheria, kwa kuwa vyama au wagombea wanaoshindwa kutimiza sheria
hiyo watachukuliwa hatua ikiwemo kupelekwa makahamani ambako
wakipatikana kwa upande wa Chama kitafungiwa kushiriki uchaguzi wowote
utakaofuatia na kwa upande wa wagombea mhusika atatozwa faini ya sh.
milioni 2, au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote pamoja.
Kulingana na Sheria ya Uchaguzi, chama kinatakiwa kisitumie ghara
inayozidi sh. bilioni 17, na kikilazimika kuzidi kiwango hicho kisididi
zaidi ya asilimia 15 ya kiwango kinachotakiwa, huku kwa upande wa
wagombea kiasi kinachotakiwa ni sh. bilioni saba na kwa wabunge sh.
milioni 33 hadi 88 kulingana na mazingira ya jimbo.
No comments:
Post a Comment