WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mkutano wa kimataifa uliojadili jinsi ya
kupambana na rushwa duniani ni kiashiria tosha kwamba tatizo la rushwa
ni kubwa sana na linataka juhudi za pamoja katika kukabiliana nalo. (It’s a serious graft that needs concerted efforts).
Ametoa
kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Waziri wa Nchi wa
Uingereza anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa, Bibi Justine
Greening walipokutana kwenye mkutano huo uliofanyika Lancaster House,
jijini London, Uingereza.
Waziri
Mkuu ambaye alihudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe
Magufuli, alimweleza Bibi Greening kwamba viongozi wa Serikali wa awamu
ya tano wameamua kwa dhati kupambana na kila ovu linalotokana na janga
la rushwa na pia wameamua kuwajibika na kuachana na tabia ya kufanya
kazi kwa mazoea.
“Sasa
hivi nchi yetu ina utamaduni mpya wa kufanya kazi na tumeamua kufanya
kazi kwelikweli na siyo tena kwa mazoea, tumeamua kuweka utamaduni mpya
wa kupiga vita rushwa ili kuleta uwajibikaji na uwazi miongozi mwa watu
wetu,” alisema.
Alipoulizwa
ni kitu kimechangia kufanya Tanzania ing’are kimataifa katika vita hii,
Waziri Mkuu alijibu kwamba Tanzania imetumia mambo manne ambayo ni
kuzuia rushwa isitolewe ama kupokelewa (prevention), kampeni za
kuelimisha jamii, kufanya mapitio ya sheria na kuwepo kwa utashi wa
kisiasa.
“Serikali
inachukua hatua za kiutawala na kisheria kama vile kuanzisha mahakama
maalum ya mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi mwezi Julai mwaka
huu,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa
upande wake, Bibi Greening alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali
ya awamu ya tano katika kupambana na rushwa na kwamba ndiyo maana
Tanzania ilipewa mwaliko maalum wa kushiriki mkutano huo kwa vile baadhi
ya mataifa yanaziona juhudi zinazofanywa na Serikali.
Pia
alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa nia ambayo Serikali ya
awamu ya tano imeionyesha katika kuwa na mpango wa kuendeleza viwanda.
Pia
alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba nchi yake iko tayari kuisaidia
Tanzania kwenye mpango wake ilionao wa kupeleka umeme vijijini (Rural
Electrification Programe). “Tuko tayari kuwasiidia kutekeleza mpango huu
kupitia taasisi ya Energy Africa Initiative ambayo inapata ufadhili
kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID),” alisema.
Wakati
huohuo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia
masuala ya kimataifa, Bibi Sarah Sewall ameipongeza Tanzania kwa kupiga
hatua katika mapambano dhidi ya rushwa na kusisitiza kwamba makampuni
mengi ya Marekani yana nia ya kuja kuwekeza Tanzania.
“Ninaamini
uwekezahji huu utasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa
watu wetu. Tunampongeza Rais Dk. Magufuli kwa juhudi anazofanya na
nipende kusisitiza kwamba ushirikiano baina ya Tanzania na Marekani
utaendelezwa katika maeneo yetu ya siku zote,” alisema.
Waziri
Mkuu alimshukuru Bibi Sewall na kumsisitiza asiache kusaidia kuwahimiza
wamarekani wengi waje kutalii Tanzania na wawekezaji zaidi waje
kuwekeza nchini katika nyanja mbalimbali zikiwemo uanzishaji wa viwanda,
uongezaji thamani kwenye mazao yanayozalishwa nchini na kuhakiksha kuwa
Watanzania wanajifunza teknolojia mpya na za kisasa.