Wednesday, 22 June 2016

HAKUNA MAJERUHI YANGA -MURO.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
BENCHI la Ufundi la Kikosi cha Yanga limeweka wazi kuwa hali ya beki wake wa kushoto Oscar Joshua aliyeumia katika mchezo wa kwanza wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mo Bejaia anaendelea vizuri na atarejea uwanjani tena Jumanne kukipiga na TP Mazembe huku beki wa kulia Juma Abdul anaendelea vizuri na anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi mepesi.

Abdul alikosa mechi ya awali baada ya kuwa majeruhi kwa kuumia sehemu ya kifundo cha mguu na kuukosa mchezo wa kwanza na nafasi yake ikichukuliwa na Mbuyi Twite. Hata hivyo kwa sasa anaendelea vizuri na daktari ameweka wazi kuwa anaweza kuanza mazoezi na timu itakaporejea ataungana na wenzake.

Mkuu wa Kitengo cha habari na Mawasiliano Jerry Muro (Pichani)amesema kuwa Joshua anaendelwa vizuri na watakaoukosa mchezo huo ni Beki wa kushoto Mwinyi Haji aliyepata kadi nyekundu pamoja na mshambuliaji Amisi Tambwe mwenye kadi mbili za njano alizozipata kwenye mchezo wa marudiano na Segrada Esperanca ya Angola na wa hatua ya makundi na Mo Bejaia.

"Ni wachezaji wawili tu ndiyo watakaokosa mchezo dhidi ya TP Mazembe ambao ni Mwinyi anayetumikia kadi nyekundu na Tambwe mwenye kadi mbili za njano, kwahiyo katika mchezo huo Oscar atarejea tena uwanjani na Abdul anaendelea vizuri ameanza mazoezi mepesi mepesi na pindi timu itakaporejea ataungana nao,"amesema Muro.

Kwa sasa Yanga inaendelea na mazoezi katika jiji la Antalya nchini Uturuki ikiwa inajiandaa na mchezo dhidi ya TP Mazembe ambao utapigigwa Siku ya Jumanne Juni 28 na unatarajiwa kuwa wa ushindani wa hali ya juu hasa baada ya Yanga kupoteza mchezo wao wa awali na wakihitaji matokeo na TP Mazembe wakitaka ushindi ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kuingia nusu fainali.

WAZIRI WA AFYA , MAENDELEO YA JAMII , JINSIA, WAZEE NA WATOTO ATEMBELEA VIJIJI VILIVYOKUMBWA NA MLIPUKO WA UGONJWA USIOJULIKANA WILAYANI KONDOA.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kutembelea vijiji vilivyokumbwa na mlipuko wa ugonjwa usiojulikana katika kijiji cha mwaisabe, Wilayani Kondoa.

Katika ziara hilyo ameambatana na wataalam mbalimbali ambao wameweka kambi kwenye vijiji hivyo ili kufuatilia wagonjwa majumbani.vile vile ametembelea wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya kondoa.
Mbunge wa Kondoa,Juma Nkamia akizungumza wakati wa ziara hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Kondoa Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kutembelea vijiji vilivyokumbwa na mlipuko wa ugonjwa usiojulikana katika kijiji cha mwaisabe,Wilayani Kondoa

Jeshi la Ujerumani lapanuwa operesheni yake Mediterenia

Jeshi la Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Bundeswehr, litakuwa siku za mbele linalinda sio tu mwambao wa Libya, bali pia kuwaandama wafanyabiashara haramu wa silaha. Baraza la mawaziri limekubaliana operesheni ya ukaguzi wa manuari za Umoja wa Ulaya katika Bahari ya Mediterenia, inayojulikana kwa jina la Sophia, ipanuliwe. Juhudi za kusimamia utekelezaji wa vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa zimelengwa kuwazuwia wanamgambo wa itikadi kali wa Dola la Kiislam wasipatiwe silaha katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini. Zaidi ya hayo, kwa kupanuliwa shughuli za ukaguzi za manuari za Umoja wa Ulaya, itapatikana njia pia ya kupatiwa mafunzo walinzi wa fukwe za Libya. Uamuzi wa baraza la mawaziri unabidi uidhinishwe na bunge la shirikisho, Bundestag. Hata hivyo, serikali kuu ya muungano inadhibiti wingi wa viti bungeni.

Hatima ya Umoja wa Ulaya inafungamanishwa na matokeo ya kura ya maoni ya Uingereza



Rais Francois Hollande wa Ufaransa anasema mustakbali wa Ulaya unategemea matokeo ya kura ya maoni ya Uingereza kama itasalia au itatoka katika Umoja wa ulaya. Rais Hollande amesema hayo baada ya mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico, mnamo mkesha wa kura ya maoni ambapo Waingereza watachagua kama wanataka nchi yao itoke au Brexit au isalie katika Umoja wa ulaya. Rais Hollande anasema Paris itauangalia uamuzi wa waingereza kuwa "usiobadilishika" na kuongeza "London itakumbwa na hatari kubwa ikiwa haitokuwa na njia ya kuingia katika soko la pamoja. Rais Francois Hollande wa Ufaransa alikuwa kila mara akiitetea umuhimu wa Uingereza kusalia katika Umoja wa Ulaya. Wito kama huo umetolewa pia na kansela Angela Merkel wa Ujerumani hii leo. "Bila ya shaka ninataka Uingereza iendelee kuwa mwanachama wa Umoja wa ulaya lakini uamuzi wanao wananchi wa Uingereza" amesema Kansela Merkel mbele ya maripota baada ya mazungumzo pamoja na Waziri Mkuu wa Poland, Beata Szydlo

Putin ailaumu NATO kwa "uchokozi"

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameilaumu Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa kile alichokiita "matamshi makali" na "harakati zake za uchokozi" karibu na mpaka wa Urusi. Rais Putin ameonya visa kama hivyo vitailazimisha Moscow kuimarisha nguvu zake za kijeshi. "NATO inazidisha maneno na harakati za uchokozi karibu na mipaka yetu," amesema Rais Putin mbele ya wabunge wa nchi hiyo waliokusanyika katika kumbukumbu za miaka 75 tangu Ujerumani ya zamani ya Wanazi ilipoivamia Usovieti. Rais Putin amezikosoa nchi za Magharibi kwa kukataa mchango wa Urusi kusaidia kukabiliana na adui wa pamoja ambae ni ugaidi wa kimataifa, kama walivyolipuuza onyo la Soviet Union kuhusu Hitler na kama wanavyojaribu kuitenga Moscow katika mzozo wa Ukraine. Uhusiano kati ya Urusi na nchi za Magharibi umepooza na kufikia kiwango cha vita baridi tangu Moscow ilipolikalia eneo la Crimea mwaka 2014 na kuunga mkono vuguvugu la wanaotaka kujitenga mashariki ya Ukraine.

Ibrahimovic kustaafu soka ya kimataifa


Nyota wa Sweden Zlatan Ibrahimovich ametangaza kwamba atastaafu katika soka ya kimataifa baada ya michuano ya Euro 2016.
Taifa lake linakutana na Ubelgiji katika mechi ya mwisho ya kundi E siku ya jumatanoambayo huenda ikawa mechi yake ya mwisho kwa taifa lake.
Alisema:Ninajivunia kile nilichofanikiwa kupata na kila mara nitatembea na bendera ya Sweden.
Klabu ya Manchester United imehusishwa pakubwa na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye alikuwa ajenti huru baada ya kuondoka klabu ya Paris Saint Germain ya Ufaransa .

Wachezaji wa Albania kuzawadiwa paspoti za kidiplomasia


Taifa la Albania limesema kuwa litawazawadi wachezaji wake wa soka pasipoti za kidiplomasia kwa kuishinda Romania 1-0 katika michuano ya Euro2016.
Taifa hilo halijashiriki katika mchuano wowote wa soka wenye tajriba ya hali ya juu.
Lakini haijulikani iwapo taifa hilo litafuzu kwa raundi ya pili nchini Ufaransa.
Timu hiyo itapewa zawadi zaidi ya Euro milioni moja pamoja na pasipoti hizo mpya,serikali imesema.
Albania ilipoteza mechi zake mbili na kuwa wa tatu katika kundi lake.
Waziri mkuu wa Albania Edi Rama alishuhudia furaha iliokuwepo nchini humo baada ya Armando Sadiku kufunga bao la kichwa na la ushindi dhidi ya Romania katika kipindi cha kwanza cha mechi.